Mafunzo ya Ufugaji wa Nyuki na Mazao Yake Mkoani Singida

0 Comments

UTANGULIZI

Tarehe 27 Mei 2023 Taasisi ya TUNU PINDA YOUTH FOUNDATION ilifanya ziara ya kimkakati ya kutembelea Kijiji cha Nyuki katika mkoa wa Singida-Kisaki. Kwa niaba ya uongozi wa TUNU PINDA YOUTH FOUNDATION “Kitovu Cha Elimu ya Ujasiriamali kwa Vijana” tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwa kufanikisha ziara hii kwa asilimia mia moja 100%, Zipo changamoto zilizojitokeza za kibinadamu lakini kubwa zaidi safari yetu kuwa Salama kwenda na kurudi

KUHUSU ZIARA YA MAFUNZO

Ziara yetu ya mafunzo ilikuwa ya mafanikio kedekede, tulisoma kinadharia na vitendo.Hongera sana kwenu Vijana wote hasa Walioshiriki kwa kufika Kijiji cha Nyuki Singida, maana mmeonesha ukomavu,ujasiri,uthubutu,na ari ya kupenda maendeleo. Kutoa fedha Kwa ajili ya kwenda kupata elimu ya ufugaji wa Nyuki Kwa Vijana wa kisasa ni hatua ya uthubutu wa hali ya juu. Hongereni sana mnaipa Taasisi nguvu ya kwenda hatua 1000 mbele. Wengi walikuwa wakipasikia au pengine kuona picha za Asali kwenye ma-group ya mtandao wa WhatsApp wakati wengine wakiwa hawajui kabisa. Tulianza kupata uhalisia baada ya kukiona kibao kikubwa kilichaondikwa KIJIJI CHA NYUKI CO. LTD, WHERE NATURE MADE BEES AND PEOPLE BEST FRIENDS” tulifurahishwa na kustajaabishwa na wafanyakazi kwa makumi wakiwa wanachakarika na kazi zao za nyuki, wapo wapishi, watengeneza mizinga, wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza asali, walinzi, waongoza watalii “Tour guides”,

Maafisa wa vitengo maalum kama Afya, mafunzo, miradi n.k ambapo kwa mujibu wa Mkurugenzi Kiemi kuna wafanyakazi wasiopungua 115 katika Kijiji cha Nyuki ambacho kinachukua jumla ya ekari 45,000 ambapo zipo katika Kata za Kisaki, Ikungi, Iglansoni, Itigi Mkoani Singida na Kata ya Uyui iliyopo mkoani Tabora.
Tulipata mafunzo na uelewa juu ya mazao ya Nyuki na huduma zingine katika Kijiji cha Nyuki kama ifuatavyo:

1. ASALI ASILIA(Organic Honey). UPEKEE wake ni asali ambayo ni UNCONTAMINATED (haina mchanganyiko wowote wa kitu kisichofaa, kiwango cha maji ni kidogo sana, ina harufu nzuri na maua ya mimea ambapo nyuki wameitengeneza ni Adimu na inapatikana Singida tu
2. VUMBI LA SINGIDA: (Multifloral bee pollen). Hii ni Bidhaa inayojulikana kama “Only nature complete food” au “Miracle or Magic food”. Ina protini -30-40% , Vitamini na madini yote yanayohitajika na mwili wa Binadamu. Wengi wanaitumia kama bidhaa inayoongeza nguvu za kiume na za kike, inaimarisha Kinga ya mwili ya binadamu dhidi ya magonjwa nyemelezi na kuratibu ukuaji wa Watoto. Wastani wa kuuza zao hili kwa kilo ni TZS 300’000/-
3. MISHUMAA YA NTA (Natural Air Purifiers-beewax candles). Huu ni Mshumaa ambao ni spesheli kwa kuwasha Chumbani kwa ajili ya Kusafisha hewa, kutoa Mwanga na kutoa Harufu nzuri na pia sehemu ya Matibabu ya Macho maana inakupa kitu kinaitwa “Yellow illuminate” inavutia na inanukia vizuri saana. Wastani wa kuuza zao hili kwa kilo ni TZs 15’000/-
4. SUMU YA NYUKI (Bee venom). Hii inasadikika ina peptides zinazofanana na zile ya immune system ya mwili wa Binadamu au vitu ambayo vinachangia kwa asilimia zaidi ya 80% kuimarisha Kinga ya mwili. Wastani wa kuuza zao hili kwa kilo ni TZS 180M
5. GUNDI YA NYUKI ( Propolis). Hii ni bidhaa ya nyuki ambayo ni “Strong anti-Bacteria , Anti-Fungi na Anti-viruses. Kwamba ni moja ingredient kwenye viwanda vya vipodozi na Madawa. Pia hutumika “ku-relax nerves” wakati wa Operation kubwa za kidaktari zinazohusisha kukata mishipa ya Fahamu. Wastani wa kuuza zao hili kwa kilo ni TZS 750,000.
6. MAZIWA YA NYUKI ( Royal jelly). ii bidhaa ni Anti-aging yaani Humfanya mtumiaji asizeeke mapema kwani huunganisha mwili na kuupa uimara. Wastani wa kuuza zao hili kwa lita TZS 12M.
7. SUPU YA NYUKI (BEE BROOD): Hili ni zao la nyuki ambalo ni watoto wa nyuki au larvae lina protini nyingi. Wazee wengi na wavunaji wa asali wanatafuna masega yakiwa na matoto yale pamoja. Hii kwa historia inasadikika wanaokula hivi wawaumwi maradhi mbalimbali mara kwa mara. Hii kwangu ilikuwa mara ya kwanza na nilijikaza na mwisho nikazoea. Wastani wa kuuza zao hili kwa lita ni TZS 50’000.

Mpaka hapo unaweza kuona kuna utajiri kiasi gani katika uwekezaji huu mkubwa wa nyuki na mazao yake. Vijana tuchukue hii fursa kwa ukubwa na umuhimu sana maana bado tuna mapori mengi sana ambayo hayajatumika na nyuki wanapata changamoto kubwa ya kutafuta sehemu za kutengenezea asali.

SHUKURANI:-

Kipekee tunawashukuru sana walezi wetu Waheshimiwa sana Mama na Baba Mizengo Pinda miongozo,ushauri mzuri kwetu viongozi wa TUNU PINDA YOUTH FOUNDATION na Vijana wote Kwa ujumla,Tulitamani uwepo wenu lakini Kwa sababu ya majukumu, japo Dua na sala zenu wazee wetu zilienda nasi hiyo ilikuwa faraja kwetu. Vijana wana nguvu na wanajua mbio lakini wazee wanajua njia nyinyi mnatuongoza njia vyema.

Niwashukuru viongozi wa Taasisi Mkurugenzi (Petro Paresso), Katibu Mkuu (Charles Sadalah) Mhazini (Upendo Lyimo), Kwa bidii kubwa sana hasa kulisimamia jambo hili hata kufanikiwa. Tunawashukuru sana. Tuwashukuru Washiriki wote kila mtu kwa nafasi yake kwa kusimama pia kama viongozi kuwaongoza wengine pale ambapo tulisahau kuweka sawa,Hakika tumejifunza mengi katika safari hii.

Tunawashukuru pia Wakurugenzi wa Ifoneo Kijiji Cha Nyuki, wakiongozwa na mtaalam Philemon Josephat Kiemi, almaarufu “Kiemi”. Kwa kutupokea,kutufundisha,kutulisha,kutupa zawadi ya asali kila mshiriki na Kwa kushirikiana na TPYF kutoa vyeti vya ushiriki hakika mnaonesha njia na nyinyi ni chachu ya maendeleo.

CHANGAMOTO:

Safari/Ziara hasa inayokutanisha watu haikosi changamoto, Kwa niaba ya Uongozi tuombe radhi pale ambapo tulikosea na kwenda kinyume na matarajio yenu. Tulipata changamoto ya usafiri ikiwa ni pamoja na gari tulilokodi kupata hitilafu hivyo kubadilishiwa gari nyingine tukiwa katikati ya safari. Hii ilipelekea kuchelewa kufika Singida na vile vile kuchelewa kuondoka Singida ambayo ilipelekea kuwa na muda mchache wa kujifunza zaidi na kupata uelewa wa ufugaji wa nyuki na mazao yake. Hata hivyo tunawashukuru walimu wetu na wataalamu walijitahidi kwa uwezo wao na uzoefu kutupitisha katika maeneo yote muhimu katika ujasirimali huo.

Changamoto ya kifedha

Taasisi yetu bado ni changa ikiwa tumeanza toka tumesajiliwa tuna wanachama hai saba (7) tu waliojisajili kwa ada na kiingilio ikiwa ni pamoja na waanzilishi. Ada peke yake haiwezi kukidhi mahitaji yetu japo tunahitaji kwa ajili ya kuendesha ofisi na changamoto ndogo ndogo za ofisi. Hii ilitulazimu kuchangisha japo kiasi kidogo kwa vijana ambao wapo tayari kujifunza ama kupata elimu hii japo kwa uchache wakati wanajipanga kufanya mafunzo kamili ama kujipa motisha na zaidi kujitafuta na kujipambanua katika sekta nyingine za kiuchumi kwa maendeleo yao. Tunaomba wadau nmbali mbali mpatapo nafasi ya kutushauri milango iko wazi lakini pia kwa watakaojaliwa chochote wanaweza kuchangia kupitia

Akaunti ya Taasisi: 52010104014 (NMB)

Jina la Akaunti; Tunu Pinda Youth Foundation